WALIMU wanaofundisha darasa la sita katika shule za msingi mkoani Mbeya wameishutumu Wizara ya Elimu na mafunzo ya Ufundi kwa kuchelewesha kitabu cha kiada hali ambayo inawapa ugumu katika ufundishaji.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti walisema “wizara iliamua kila darasa liwe na vitabu vya kufundisha visivyozidi viwili lakini darasa la sita peke yao hawana kitabu hicho cha kiada hali ambayo inatupa ugumu wa sisi walimu kufundisha na inaweza kumfelisha mwanafunzi aingiapo darasa la saba”.
Waliongeza kuwa licha ya kuwa na muhtasari wa masomo ya darasa hilo lakini wanakabiliwa na changamoto ya vitabu vya ziada ambapo shule za msingi hazina maktaba zitakazoweza kuwasaidia kuandaa masomo kulingana na muhtasari wa somo husika.
“hakuna umuhimu wa kuwa na muhtasari kwani maktaba hakuna na kama ipo basi ipo mkoani na kama tukiamua walimu wote twende hatutatosha sasa ufundishaji unakuwa mgumu na ndio maana tunaiomba wizara husika ituletee vitabu cha kiada haraka ili viturahisishie kazi”.
Afisa elimu wa mkoa wa Mbeya Juma Kaponda alisema kitabu cha kiada kwa ajili ya darasa la sita kipo njiani kwa madhumuni ya kumrahisishia mwalimu kazi ya kufundisha na kimechelewa kwasababu ya wadau ambao ni wananchi walipewa uhuru wa kuandika vitabu kwa kufuata muhtasari sasa vimekuwa vingi hivyo wizara imekaa chini kuchambua vitabu viwili bora katika vitabu vya wadau walivyovileta”.
Kaponda aliongeza kuwa kitu cha muhimu kwa mwalimu ni muhtasari hivyo ugumu unaojitokeza ni kutokana na ukosefu wa maktaba katika kila shule hasa ukizingatia mkoa wa mbeya una shule za msingi 1059 ambazo asilimia 98 hazina maktaba.
No comments:
Post a Comment