Saturday, May 22, 2010
SERIKARI YAHAHA UCHAGUZI OCTOBA 2010
Mwanannchi Newspaper
Rais Jakaya kikwete akiongoza kikao cha kamati kuu ya CCM kilichofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam jana kujadili mchakato wa uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
KATIKA kile kinachoonekana ni kujipanga vema na kujihami kwa maswali magumu wakati wa kampeni za uchaguzi, Ikulu imetoa waraka wa kuzuia mawaziri kusafiri nje na badala yake kuwaagiza kuzunguka mikoani kuelezea mafanikio ya serikali ya awamu ya nne.
Waraka huo, ambao umepewa jina la "Mlitutuma, Tumetekeleza, Tumerudi Kuwaelezeni Tulivyotekeleza na Kuwasikilizeni", pia unawaagiza mawaziri kukutana na watu wa aina mbalimbali kwenye ziara hizo, wakiwemo viongozi wa dini na viongozi wa vyama vya wafanyakazi.
Hii itakuwa ni mara ya tatu kwa Ikulu kutoa maagizo kama hayo baada ya ziara ya kwanza iliyofanywa mwaka 2007 ya kutetea na kuelezea bajeti ya mwaka 2007/08, ambayo ilikuwa ya kwanza kwa serikali ya awamu ya nne, kuhusishwa na ubadhirifu wa fedha za walipakodi na kampeni za mawaziri kupata ujumbe kwenye halmashauri kuu ya CCM, chombo ambacho ni cha pili kimamlaka kwenye chama hicho kikongwe baada ya mkutano mkuu.
Pia katika ziara hizo, mawaziri walijikuta wakiishia kufanya vikao vya ndani ya chama kutokana na wananchi kuwazomea kila walipotaka kufanya mikutano.
“Huko nyuma, tumepata kuwaandalia Outreach Programmes angalau mara mbili. Zote mbili zilianza vizuri lakini zikaishia njiani kabla ya kumalizika,” inasema sehemu ya waraka huo.
“Ili kuhakikisha kila waziri anatekeleza wajibu wake katika hili, tunashauri ziara zote za mawaziri za nje ya nchi zisimamishwe hadi kila waziri atakapokuwa amefanya ziara yake.”
Waraka huo umetolewa wakati Rais Jakaya Kikwete akiwa amewatangazia vijana, viongozi na wana CCM wote kujiandaa kujibu tuhuma za ufisadi ambazo zitaibuliwa na wapinzani kama silaha kwenye kampeni za uchaguzi wa Oktoba.
Agizo hilo la Kikwete alilolitoa juzi mjini Iringa wakati akifunga mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM ( UVCCM), limedhihirishwa na waraka huo ambao umeambatana na ratiba ambayo inaonyesha ziara za mawaziri hao mikoani kueleza wananchi mafanikio ya serikali katika kutatua kile walichoituma.
Katika waraka huo wa Mei 11, Ikulu imeelekeza na kutoa mapendekezo ya wadau husika ambao kila waziri atapaswa kukutana nao katika mikutano yake mikoani kwa mujibu wa ratiba.
Waraka huo, ambao Mwananchi imeona nakala yake, umeelekeza kwamba katika mkutano wa kwanza waziri atapaswa kukutana na wafanyakazi wa serikali, viongozi wa dini, viongozi wa serikali za mitaa, madiwani, wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi na wawakilishi wa CCM.
Agizo hilo la waraka limetaja wadau wengine wakuu wanaopaswa kukutana na mawaziri kuwa ni pamoja na wajumbe wa nyumba kumi, wawakilishi wa sekta za wizara zilizopo mkoani humo, wawakilishi kutoka sekta ya biashara mkoani na wawakilishi wa sekta nyingine za uchumi.
Sehemu ya waraka huo ambao unatokana na maamuzi kati ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais (Ikulu) na wasemaji wa wizara za serikali, imetoa pia ratiba ambayo kila waziri atapaswa kutembelea mkoa mmoja kwa tarehe maalum iliyopangwa.
“Inapendekezwa katika programu hii kila waziri atembelee mkoa mmoja kwa tarehe zilizopangwa...,” inaeleza sehemu ya waraka huo.
Waraka huo umeelekeza madhumuni mawili ya ziara hizo ambayo ni pamoja na kila waziri kueleza mafanikio ya wizara yake katika miaka mitano ya uongozi wa serikali ya awamu ya nne na kusikiliza kero na shida za wananchi katika maeneo wanayotembelea na kujibu hoja.
Ikulu imeeleza katika waraka huo ikisema: “Kabla na baada ya ziara ya waziri, kila wizara itatakiwa kufanya mambo yafuatayo, kutengeneza vipindi maalumu viwili in the form of Documentaries (katika mfumo wa vipindi vya makala (redio na TV)).”
Kazi nyingine kwa mujibu wa waraka huo ni pamoja na “kuandaa tangazo fupi (public service announcement) kutangaza mafanikio ya wizara katika miaka hiyo mitano kwa ajili ya redio na televisheni na matangazo hayo yaanze kutumika mara moja".
Pia wametakiwa "kuandaa retreat na wahariri wakuu na wahariri waandamizi wa vyombo vya habari nchini kwa nia ya kujenga uhusiano na vyombo hivyo na pia kuwaelezea wahariri hao mafanikio ya serikali ya awamu ya nne".
“Kabla ya kuanza ziara, kila waziri aandae mkutano mkubwa wa waandishi wa habari kuelezea mafanikio na shabaha ya ziara yake,” unaeleza waraka huo.
“Aidha, Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu inapendekeza kuwa ofisi zote za wakuu wa mikoa zifuatilie ratiba hiyo ili kuandaa na kufanikisha mikutano hii na waziri husika.
“Pia taarifa kwa vyombo vya habari iandaliwe kabla ya kuanza na ratiba nzima ya waziri na mkoa itolewe kwa wana habari.”
Ratiba ya ziara iyo inaonyesha, mawaziri Muhammad Seif Khatibu (Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano) alipaswa kuanza ziara mkoa wa Dar es Salaam kuanzia Mei 13 hadi 16, 2010, William Ngeleja (Waziri wa Nishati na Madini) alipaswa kuanza ziara mkoa wa Shinyanga (Ziara ya kwanza) kuanzia tarehe hiyo, Profesa David Mwakyusa (Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii) naye alipaswa kuanza ziara mkoani Arusha katika muda huo (ziara ya kwanza).
Waziri mwingine ambaye alipaswa kuanza ziara katika tarehe hiyo ni Mustafa Mkulo (Waziri wa Fedha na Uchumi), ambaye alipaswa kuwa mkoani Lindi.
Kundi la pili ambalo limetajwa katika ratiba hiyo linajumuisha mawaziri John Magufuli (Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi) ambaye alipaswa kuanza ziara mkoani Mara kuanzia Mei 17 hadi 20, 2010.
Wengine ambao wamepangiwa katika tarehe hiyo ni Dk Diodaurs Kamala (Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki) ambaye alipaswa kuwa mkoani Ruvuma, Sophia Simba (Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora) ambaye alipaswa kuwa mkoani Tanga na Profesa Jumanne Mghembe (Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi) ambaye alipaswa kuwa mkoani Iringa, katika tarehe hiyo.
Kundi la tatu ambalo limetajwa kwenye ratiba ya waraka huo linahusisha mawaziri Bernard Membe (Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa) ambaye kuanzia Mei 21 hadi 24, 2010 atapaswa kuwa mkoani Morogoro, Mathias Chikawe ( Waziri wa Sheria na Katiba) ambaye atapaswa kuwa mkoani Rukwa, Philip Marmo (Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Bunge) atapaswa kuwa mkoani Singida.
Waraka huo umeeleza kuwa kundi la nne litamjumuisha Profesa Juma Kapuya (Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana), ambaye kuanzia Mei 25 hadi 28, atapaswa kuwa mkoani Mwanza, wengine ni Stephen Wassira (Kilimo, Chakula na Ushirika) ambaye atapaswa kuwa mkoani Tabora.
Katika ratiba ya tarehe hiyo, Lawrence Masha (Mambo ya Ndani) atapaswa kuwa mkoani Kagera na Shamsa Mwangunga (Maliasili na Utalii) atapaswa kuwa mkoani Arusha (mara ya pili).
Kundi la tano, kwa mujibu wa ratiba hiyo, litamuhusisha Profesa Mwandosya (Waziri wa Maji na Umwagiliaji) kuanzia Mei 29 hadi Juni mosi, atapaswa kuwa mkoani Dodoma, Celina Kombani (Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Tamisemi) atapaswa kuwa mkoani Shinyanga (mara ya pili), Prof Peter Msolla (Mawailiano, Sayansi na Teknolojia) atapaswa kuwa mkoani Kilimanjaro.
Kundi la sita ambalo limetajwa katika ratiba hiyo, litahusisha mawaziri, Dk Hussein Mwinyi (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) ambaye atapaswa kuwa mkoani Mtwara kuanzia Juni 2-5, George Mkuchika (Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo) ambaye atapaswa kuwa mkoani Mwanza, Dk Shukuru Kawambwa (Miundombinu) atapaswa kuwa mkoani Manyara, Magaret Sitta (Maendeleo ya Jamii, Jinsi na Watoto) atapaswa kuwa mkoani Mbeya na John Chilligati (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi) atapaswa kuwa mkoani Kigoma.
Utaratibu huu uliwahi pia kutumiwa wakati wa bajeti ya kwanza ya serikali ya awamu ya nne, ambayo mawaziri walitawanywa mikoani kuinadi na kuitetea.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment