Saturday, May 22, 2010
MWINYI: KWANINI UFISADI UNAKISTHIRI SERIKALI YA NNE
RAIS mstaafu wa awamu ya pili, mzee Ali Hassani Mwinyi, maarufu kama Mzee Ruksa ameshangaa kukithiri kwa rushwa katika utawala wa awamu ya nne ikilinganishwa na tawala zote zilizopita.
Hadija Jumanne
Mzee Ruksa alisema hayo jana jijini Dar e Salaam katika mahafali ya 12 ya Chuo cha Teknologia ya Habari (IIT) alikoalikwa kama mgeni rasmi.
Alisema kuwa miongo miwili iliyopita, akiwa madarakani kama rais wa awamu ya pili rushwa ilikuwa haipo na ilikuwa haina nafasi.
Mwinyi alibainisha kwamba, wakati anatangaza ruksa kwa kila kitu hapakuwa na rushwa wala mianya yake.
“Kipindi mimi niko madarakani miongo miwili iliyopita, rushwa ilikuwa haipo na hata wakati natangaza kila kitu ruksa katika serikali yangu, kulikuwa hakuna mifuko ya rushwa serikalini wala katika sekta binafsi,” alisema Mwinyi.
Alisema anashangaa kuona rushwa inakithiri katika serikali ya awamu ya nne (ya rais Jakaya Kikwete) huku mianya yake ikizidi kuongezeka kwenye taasisi za umma na sekta binafsi.
“Inashangaza kuona rushwa imeota mizizi katika sekta mbali mbali hapa nchini kitu ambacho kinakwamisha na kudumaza maendeleo ya nchi,”alieleza Mwinyi.
Rais huyo mstaafu aliwataka vijana waliohitimu katika chuo hicho wakatumie ujuzi walioupata kujiajiri na siyo kusubiri kuajiriwa au kupata nafasi serikalini.
Aliwataka pia kuwa wapambanaji wa rushwa ambayo imeota mizizi katika sekta mbalimbali nchini.
Alipoingia madarakani miaka mitano, iliyopita Rais Kikwete aliahidi kuwa serikali yake itaongeza kasi ya mapambano dhidi ya rushwa na kwamba, atafanya hivyo kisayansi kwa kushambulia kiini chake.
“Kwa kadri mapato ya Serikali yanavyoongezeka, ndivyo tutakavyoongeza mishahara na kuboresha maslahi ya watumishi wa umma ili kupunguza vishawishi vya rushwa. Tutaendelea pia kuongeza uwazi katika maamuzi ya Serikali. Tutaimarisha uwezo wa kifedha na kiutendaji wa taasisi zilizo mstari wa mbele kwenye vita dhidi ya rushwa, hasa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Jeshi la Polisi na mahakama. Lakini yote hayo ni bure iwapo wananchi hawatajitokeza kusaidia vyombo hivyo," alisema Kikwete.
Kikwete alisema hayo Desemba 30, 2005 wakati akihutubia Bunge kwa mara ya kwanza mara baada ya kuapishwa kuwa Rais wa nne wa Tanzania na kuomba ushirikiano kutoka kwa wananchi kwenye mapambano hayo.
"Naomba ushirikiano huo kutoka kwa wananchi,” alisema Kikwete na kuongeza kuwa mbali ya hayo, alibainisha kuwa katika kupambana na rushwa ataangalia kwa ukaribu suala la mikataba.
Alieleza kuwa serikali yake inakusudia kuangalia upya taratibu za mikataba mbalimbali inayoingiwa na serikali, mashirika ya umma na idara zinazojitegemea kwa nia ya kuongeza uwazi na uwajibikaji.
Mikataba ni mwanya mkubwa wa rushwa, hasa zile kubwa. Hata hivyo, katika juhudi za serikali ya awamu ya nne kupambana na rushwa, kesi mbalimbali za rushwa kubwa zinazofikia 25 zipo mahakamani.
Aidha, mwaka huu serikali imerekebisha sheria na kuipa meno Takukuru ili kuipa nguvu zaidi ya kupambana na tatizo hilo, na kidhinisha sheria mpya ya gharama za uchaguzi inayolenga kudhibiti na matumizi ya fedha haramu katika uchaguzi.
Katika mahafali hayo, Mwinyi alitoa shahada ya kwanza, stashahada na stashahada na digrii kwa wahitimu 150 katika masomo ya teknolojia ya habari, biashara na kompyuta.
Wahitimu 15 kati ya 150 ambao walichukua shahada ya teknologia ya habari walitunukiwa tunzo maalum baada ya kufanya vizuri katika masomo hayo.
Wahitimu wengine 50 pia walitunukiwa tuzo katika masomo stashahada na wengine 85 stashahada ya kompyuta na biashara.
Chuo hicho kilianzishwa Mei 1990 chini ya jina Microtek Computers Limited kabla ya kubadilishwa mwaka 1992 na kuwa Taasisi ya Teknologia ya Habari(IIT).
Mkurugenzi mkuu wa Taasisi hiyo Mujtaba Salemwalla, alisema kuwa elimu hiyo waliyopewa vijana hao hawana budi kuitumia ipaswavyo kwani wamebeba jukumu la kuihudumia jamii.
Chuo hicho kwa sasa kina matawi mawili katika jiji la Dar es Salaam, katika jengo la Kelvin lililopo mtaa wa Samora na katika jengo la Africab Tower barabara ya Kawawa karibu na Machinga Complex na kinatoa shahada na stashahada.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment