Na Keneth Goliama,Mbeya.
MKAZI wa Kijiji cha Kakozi wilayani Mbozi Mkoani Mbeya, aliyefahamika kwa jina la Bernad Cheyo (70) juzi majira ya saa 9:00 alasiri alikutwa ameuawa na watu wasiojulikana kwa madai ya kujihusisha na uchawi.
Habari kutoka eneo la tukio zilisema kuwa watu wasiojulikana walimvamia marehemu na kumwua na mwili wake kuutupa pembezoni mwa njia iendayo nyumbani kwake mita zipatazo 500 kutoka mahali anapoishi.
Mashuhuda waliongeza kuwa siku ya tukio walikuwa naye klabu ya pombe za kienyeji ambako alikuwa akipata kinywaji na mara baada ya kumaliza waliagana naye na kila mmoja alienda nyumbani .
Mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa na jeraha moja kubwa shingoni upande wa kushoto linalosadikika lilitokana na kupigwa na kifaa chenye ncha kali.
Hata hivyo hapo awali inasadikika alikuwa akijuhusisha na vitendo vya kishirikina na watu waliomuua wametajwa majina yao kuwa ni Leonard Silavwe, Mawazo Sinkala na mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Sinkala ambao wote hawajulikani waliko.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Advocate Nyombi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na wahusika wanatafutwa na Jeshi la Polisi mkoani humo.
MKAZI wa Ikuti-Iyunga Hassan anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 30 hadi 35, alifariki wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Mbeya baada ya kupigwa na wananchi wenye hasira kwa kosa la kuiba masandukun ya kiwanda cha bia (TBL).
Walioshuhudia tukio hilo walisema kuwa marehemu akiwa na wenzake wawili walivunja na kuiba masanduku ya chupa za bia tupu katika kiwanda cha kutengenezea bia (TBL) majira ya saa 5:00 usiku, ambapo thamani ya masunduku haikujulikana mara moja.
Waliojeruhiwa katika tukio hilo, Amoni Damiani(31) mkazi wa Inyara-Iyunga na Nestory Mgaya(22) mkazi wa Nzovwe Jijini humo, ambao wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa huku wakiwa chini ya Ulinzi wa Polisi na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali hiyo.
Wakati huo huo Mpanda baiskeli mkazi wa kijiji cha Lunwa, wilayani Mbarali aliyefahamika kwa Fabian Mbikise(23) alikufa papo hapo baada ya kugongwa na gari lenye namba T 666 BCR, Yutong majira usiku lililokuwa likiendeshwa na Mfaume Hamad katika barabara ya Mbeya-Iringa.
Hata baada ya Kufuatia tukio hilo dereva wa basi hilo alikimbia na kulitelekeza basi hilo ambalo hata hivyo liliendeshwa na dereva wa pili ambaye hakufahamika mara moja na kufikishwa katika kituo cha polisi.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Mbeya Advocate Nyombi alithibitisha kutokea kwa matukio yote.
Mwisho
No comments:
Post a Comment