Photobucket

Wednesday, April 21, 2010

WALUTHERI WALUHUSU NDOA ZA MASHOGA

Tanzania Daima

na Mwandishi Wetu, STOCKHOLM , Sweden

KANISA la Kiinjili la Kilutheri lenye waumini wengi zaidi nchini hapa, limekubali kubariki ndoa za watu wa jinsia moja.
Sweden, imekuwa ni nchi ya kwanza duniani kuruhusu mashoga kuoana ndani ya kanisa hilo kubwa duniani.
Hatua ya kanisa hilo imekuja ikiwa ni miezi mitano tu baada ya serikali ya hapa kulifanya suala la watu wa jinsia moja kuoana kuwa la kisheria.
Karibu asilimia 70 ya wakuu 250 wa kanisa hilo , walipiga kura kuunga mkono kuruhusu watu wa jinsia moja kuoana ndani ya Kanisa la Kilutheri.
Taarifa ya kanisa hilo ilieleza kuwa, hatua hiyo itaanza kutekelezwa kuanzia Novemba 1.
Kanisa la Lutheran limejiunga na imani nyingine chache duniani zinazokubaliana na ndoa za jinsia moja.
Nchini hapa, kati ya watu wanne, watatu kati yao ni waamini wa dhehebu la Kilutheri. Kwa maana hiyo, robo tatu ya raia wa nchini hapa ni waumini wa dhehebu hilo , japo idadi ya wanaohudhuria ibada imepungua sana .
Kanisa la Kilutheri nchini hapa, ambalo lilikuwa likiongoza nchi hadi mwaka 2000, linaungana na Bunge ambalo lilipitisha sheria ya kuruhusu watu wa jinsia moja kuoana, ambako utekelezaji wa sheria hiyo ulianza rasmi Mei 1, mwaka huu.
Hata hivyo, baada ya Bunge kupitisha sheria hiyo, maamuzi ya wakuu wa kanisa hilo kuruhusu ndoa za jinsia moja yalichukua muda.
Sweden pia imefungua milango yake ya kuruhusu wanandoa wa jinsia moja kupata haki ya kuasili watoto.
Makanisa madogo nchini hapa ya Orthodox na Roman Catholic yalieleza kusikitishwa na maamuzi hayo ya Kanisa la Kilutheri.
Katika taarifa yao ya pamoja, kiongozi wa Kanisa Katoliki nchini hapa, Fredrik Emanuelson na ofisa mwandamizi wa Kanisa la Orthodox, Misha Jaksic walisema: “Kwa masikitiko tumejifunza uamuzi wa viongozi wa kanisa la Sweden .
“Katika makanisa yetu na waamini, hatutaruhusu ndoa za jinsia moja, kwamba mtazamo huo unapigana na tamaduni na malengo ya uanzishaji makanisa.”
Wakati Kanisa la Kilutheri likifikia hatua hiyo, Kanisa la Anglikana lipo katika hatari ya kusambaratika baada ya kutokea mgawanyiko mkubwa kutokana na baadhi ya nchi waamini wa kanisa hilo kuruhusu usimikaji wa wachungaji mashoga.
Ingawa kulikuwa na ripoti kuwa viongozi wa juu wa Kanisa la Anglikana nchini Marekani walikubaliana kusimamisha usimikaji wa wachungaji mashoga ili kuzuia mgawanyiko katika kanisa hilo , hivi sasa kanisa hilo lipo katika ubishani mkali usiokwisha, huku baadhi wakipinga kuruhusu ndoa za jinsia moja ndani ya kanisa na hivyo kusababisha mgawanyiko mkubwa.
Makanisa mengi ya Anglikana katika nchi za Afrika yalitishia kujiondoa katika ushirika huo wa dunia nzima baada ya kusimikwa askafu shoga zaidi ya miaka mitano iliyopita.
Kwa upande wake, Kanisa Katoliki ambalo haliruhusu hata makasisi wake kuoa, linapinga vikali ndoa za jinsia moja.
Kiongozi wa kanisa hilo duniani, Papa Benedict XVI amekuwa akilaani ndoa za watu wa jinsia moja.
Papa amekuwa akishambulia vikali kile alichokiita “uhuru wa vurugu” wa mtindo wa kisasa wa watu wa jinsia moja kufunga ndoa.

No comments:

Post a Comment