Photobucket

Saturday, April 3, 2010

US$ 30 MILION KUINUA KILIMO KWANZA TANZANIA



Dola milioni 24 za Kimarekani zatolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) kuisaidia serikali ya Tanzania ili kutekeleza kauli Mbiu ya “KILIMO KWANZA” kwa msimu wa mwaka 2009/10.



Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha na Uchumi Mustafa Mkulo wakati akifungua mkutano wa Baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Fedha na Uchumi Desemba 16, mwaka huu mkoani Mbeya.



Ameendelea kusema kuwa dola milioni 160 za Kimarekani zinahitajika ili kuhakikisha upatikanaji wa chakula kwa mwaka mzima bila matatizo yoyote.



Pia amethibitisha kuwa mkono wa Benki ya Dunia (WB) upo kusaidia jamii ya Kitanzania kutokana na athari za kuporomoka kwa uchumi duniani hususani katika nchi zinazoendelea kama Tanzania.



Katika kuhakikisha “KAULI MBIU” hiyo inatekelezwa vizuri na kwa umakini mkubwa Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni 40 ili kupunguza upungufu wa bei katika msimu huu wa zao la pamba pia kuboresha na kupanua mifuko ya kudhamini mikopo ikijumuisha “Export Credit Guarantee Scheme na “Small and Medium Enterprises Scheme”



Akizungumza kuhusu suala la Ghala la Taifa la Chakula amesema kiasi cha shilingi Bilioni 141 kimetengwa kwa ajili ya kuboresha uzalishaji na upatikanaji wa zana za kilimo.



Akichanganua zaidi amesema katika kiasi hicho shilingi bilioni 60 zimetumika katika kuboresha uzalishaji wa chakula na kununulia pembejeo za kilimo.



Aidha amesema Wizara yake itatengewa asilimia 10 ya Bajeti ya serikali ya mwaka 2010/11 kwa ajili ya sekta ya Kilimo.



Kiasi cha shilingi Trilioni 1.7 kimetolewa katika bajeti ya Serikali ya mwaka 2009/10 kwa ajili ya kunusuru uchumi wa Tanzania.



Mkutano wa baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Fedha na Uchumi ambao umeenda sambamba na kutembelea chemichemi ya Maji ya Moto iliyopo mkoani hapa unatamatishwa leo usiku kwa hafla ya pamoja katika ukumbi wa Mkapa uliopo Jijini Mbeya

No comments:

Post a Comment