Makamba adai makada wanalipwa na mafisadi
na Tanzania Daima
MASHAMBULIZI ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) dhidi ya Rais Jakaya Kikwete kuhusu udhaifu wake wa uongozi, yameleta sokomoko katika chama hicho, na sasa Katibu Mkuu, Yusuf Makamba, ameibuka na kudai wanaomtuhumu rais wanalipwa na mafisadi.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa simu jana, Makamba alidai tuhuma dhidi ya Kikwete zinatolewa na watu wenye visasi, walioshindwa uchaguzi, na ambao wanafadhiliwa na matajiri wale wale wanaoitwa mafisadi wa CCM.
“Unasema tumekumbatia mafisadi. Wanaosema CCM imekumbatia matajiri wako kwenye lisiti ya kulipwa mishahara na hao hao matajiri, kwani hili ni siri? Mbona tunayajua haya,” alisema.
Aliwataja kwa majina baadhi ya makada wa CCM ambao aliwashutumu, wakiwamo Mateo Qares na Mussa Nkhangaa, ambao juzi walitoa kauli nzito wakitaka Rais Kikwete asigombee tena urais mwaka kesho kama atashindwa kuwashughulikia wafanyabiashara mafisadi waliomzunguka.
Kauli zinazofanana na hii zilitolewa na makada wengine waandamizi katika CCM, wakiwamo Joseph Butiku, Joseph Warioba, Salim Ahmed Salim, Nape Nnauye, Dk. Harrison Mwakyembe, Fred Mpendazoe na wengine walioshiriki kongamano la siku tatu lililoandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere mapema wiki hii, kujadili mustakabali wa taifa.
Wakati Warioba na Dk. Salim wamewahi kunukuliwa wakisema nchi inapoteza mweleko kwa kukosa uongozi thabiti, kauli ambazo zimerudiwa wiki hii katika kongamano hilo, Butiku alisema rais amezungukwa na wezi, huku Qares akisema si lazima rais apewe mihula yote miwili kama ameshindwa kazi.
Akijibu tuhuma hizo, Makamba alidai zimejengwa katika misingi ya chuki kwani wengi wa makada wa chama hicho waliokuwa wakizungumza katika kongamano hilo, ama wao wenyewe au wagombea wao waliangushwa katika harakati zao za kisiasa huko nyuma.
Alisema Qaresi alikuwa mkuu wa mkoa na mgombea ubunge wa chama hicho, lakini sasa amepoteza hata nuru kwao baada ya kushindwa.
“Qaresi alikuwa mkuu wa mkoa na alikuwa na mgombea wa chama hiki, wewe unamjua, amepoteza hata nuru kwao baada ya kushindwa katika ubunge.
“Wako matajiri wangapi? Mbona aliposhindwa ukuu wa mkoa amekwenda kiwanda cha mbolea na kuajiriwa na tajiri?…Wanasema Kagoda, unawaeleza ni nani? Thibitisha. Ukisema makamba afumaniwa thibitisha.
“Sisi ni watu wazima, tuna maeneo ya kujua. Kwa hiyo sishtuki wanaposema akina Nkhangaa na Qaresi. Kama umesoma taarifa ya Redet (Taasisi ya Utafiti ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam) na ile taasisi nyingine (Synovate Tanzania) wameonyesha CCM na rais anakubalika.
“Nkhangaa ameshindwa katika kura za maoni na (Mohammed) Dewji kule Singida mwaka 2005 na inajulikana hakumtaka Jakaya, alikuwa na mgombea wake katika nafasi ya urais. Mgombea wake alishindwa. Kwa hiyo maneno haya yote ni ya chuki,” alisema.
Pamoja na mambo mengine, Makamba alisema CCM imeshinda katika uchaguzi wa serikali za mitaa kwa 93% na katika ushindi huo hawakupigiwa kura na matajiri bali na watu wa ngazi ya chini.
“Unaposema hivyo unakosea, ukishinda uchaguzi kwa asilimia 93 maana yake aliyekufanya ushinde ni chama na rais mwenyewe kama Redet anavyosema rais anakubalika kwa asilimia 83. Hiyo ndiyo indiketa ya mwaka 2010. Ni nani kama Jakaya? Hilo si la siri kila mtu anajua,” alisema Makamba.
Pamoja na Makamba, Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz ambaye ni mmoja wa wafanyabiashara wanaohusishwa kwa ukaribu na Rais Kikwete, na ambaye amekuwa akihusishwa na kashfa nyingi, ameendelea kung’ang’ania hoja yake ya kutaka liundwe jopo la majaji kuchunguza kashfa ya Richmond anayohusishwa nayo.
Alipinga kauli ya Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe aliyeshauri uwepo mjadala wa wazi katika vyombo vya habari na hukumu ya umma.
“Inatia aibu na kushangaza kumuona Dk. Mwakyembe ambaye anapenda aonekane kuwa mwanasheria aliyebobea, leo hii anakataa pendekezo langu la kuwa na timu ya majaji wanaoheshimika, ili wabaini ukweli wa madai ya kamati iliyoongozwa na yeye,” alisema Rostam.
Juzi, Dk. Mwakyembe alipendekeza wafanyabiashara wanaotuhumiwa wanunue muda katika vyombo vya habari, ufanyike mjadala wa kitaifa kati ya mafisadi na wapambanaji wa ufisadi, halafu baada ya hapo washiriki wote wapite mitaani kwa miguu kupima maoni ya umma.
Rostam, mmoja wa watu walioguswa na sakata la Richmond, hakubaliani na pendekezo hilo, na anapinga maazimio ya Bunge linaloitaka serikali iwashughulikie watuhumiwa wote wa Richmond.
No comments:
Post a Comment